BARAZA LAPITISHA MAPENDEKEZO YA BAJETI YA 2026/2027 BILLIONI 77.
BARAZA LAPITISHA MAPENDEKEZO YA BAJETI YA 2026/2027 BILLIONI 77.
Na,Mwandishi wetu.
Baraza la wafanyakazi la Wakala wa Mbegu za kilimo ASA limepitisha mapendekezo ya bajeti ya mwaka 2026/2027 shingi bilioni 77.042.
Akisoma mapendekezo hayo mbele ya baraza la wafanyakazi, Kaimu Mkurugenzi wa Huduma za Taasisi Bi. Mary Machaku amesema ASA inapanga kukusanya na kutumia kiasi Cha shilingi 77,042,398,384 kwa ajili ya matumizi ya mishahara, miradi ya maendeleo na makusanyo ya mapato ya ndani.
Machaku ametaja vipaumbele vya Bajeti hiyo ni pamoja kuzalisha tani 17,632 za mbegu ya Mahindi kwenye eneo la hekta 6,404, tani 5,108 za mbegu za Mpunga kwenye eneo la hekta 1,486, tani 412 za mbegu ya Maharage kwenye eneo la hekta 516.
Aliongeza kuwa tani 1,907 za mbegu za Alizeti zitazalishwa kwenye eneo la hekta 2,384 na tani 1,100 za mbegu za Ngano kwenye eneo la hekta 440.
Kipaumbele kingine ni ujenzi wa uzio wenye mzunguko wa kilomita 158.5 katika mashamba ya Namtumbo(34km), Kilangali (22 km), Mwele (15km), Luhafwe (15km), Msungura (0.5km), Mbozi (40 km), Bugaga (10 km), Dabaga (22km) na Arusha (21km).
Aidha, kipaumbele kingine ni kusafisha eneo jipya la hekta 1,900 kwenye mashamba ya Mbozi (Hekta 600), Msimba ,(hekta 500) na Luhafwe (hekta 800).
Akifunga kikao hicho cha Baraza la wafanyakazi wa ASA kwa niaba ya Mtendaji Mkuu Bwn. Leo Mavika , Mkurugenzi wa maendeleo ya Biashara Dkt. Basil Msuha amesema ASA itaendelea kuzalisha mbegu bora za kilimo kupitia wakulima wa mkataba na kuhimiza ushirikiano.
Msuha amesema kupitia bajeti hii ASA imejipanga kupeleka mbegu sokoni kwa wakati ili wakulima waweze kwenda vizuri na msimu wa kilimo.
Amewataka wajumbe wa baraza hilo kuwahimiza watumishi kufanya kazi kwa kujituma ili kuweza kuongeza uzalishaji wenye tija kwa jamii. Wajumbe wa baraza la wafanyakazi walipongeza bajeti hiyo na kuahidi kuitekeleza ipasavyo.
Aidha awali ya hapo Baraza hilo lilianza kwa kufanya uchaguzi mdogo kwa kumchagua katibu wa TUGHE ndugu Erick Iramba kuziba pengo lililoachwa wazi na aliyekuwa katibu wa chama hicho bwn Constantine Nzila aliyefariki dunia mwaka 2025.
