TIMU YA UFUATILIAJI NA TATHMINI (M&E) YA ASA YAPIGWA MSASA
Timu ya Ufuatiliaji na Tathmini (M&E) ya Wakala wa Mbegu za Kilimo (ASA) imepatiwa mafunzo ya siku mbili kuanzia Februari 05 hadi 06, 2026 jijini Dodoma, yenye lengo la kujengewa uwezo katika utekelezaji wa shughuli za ufuatiliaji na tathmini ya kazi na miradi ya Taasisi, kupitia Programu ya Kuendeleza Kilimo na Uvuvi (AFDP).
Mafunzo hayo yamefunguliwa rasmi na Mtendaji Mkuu wa ASA, Bw. Leo Mavika, ambaye amewasisitiza washiriki kuyazingatia kikamilifu ili kuyaweka katika vitendo na hivyo kuisaidia Taasisi kufikia malengo yake ya kimkakati.
Akizungumza wakati wa ufunguzi wa mafunzo hayo, Bw. Mavika amesema “mafunzo hayo ni muhimu kwa timu ya M&E katika kusimamia na kupima utendaji wa Taasisi, kuhakikisha thamani ya fedha kwenye miradi, kufuatilia mwelekeo wa utekelezaji wa miradi pamoja na usimamizi wa bajeti ya ASA.”
Kwa upande wake, Mkuu wa Kitengo cha Ufuatiliaji na Tathmini (M&E) cha ASA, Bw. Emmanuel Maziku, amesema mafunzo hayo ni nyenzo muhimu katika kuimarisha uwezo wa kufuatilia na kutathmini utendaji wa Taasisi, usimamizi wa kazi za Wakala pamoja na miradi inayotekelezwa.
Ameongeza kuwa mafunzo hayo yatawajengea washiriki uwezo wa kufanya ufuatiliaji na tathmini ya majukumu ya idara, vitengo na mashamba ya ASA, hatua itakayochochea na kukuza ufanisi na uwajibikaji ndani ya Taasisi.
