ASA YAKABIDIWA ENEO LA HEKTA 240 (SAWA NA EKA 601) IKIWA SHAMBA LA UZALISHAJI WA MBEGU ZA KILIMO
03 Jun, 2025
ASA YAKABIDIWA ENEO LA HEKTA 240 (SAWA NA EKA 601) IKIWA SHAMBA LA UZALISHAJI WA MBEGU ZA KILIMO

Wakala wa Mbegu za kilimo (ASA) yakabidhiwa Shamba la Mbegu za kilimo lenye Hekta 240 sawa na Ekari 601 kutoka Halmashauri ya wilaya ya Igunga kwa ajili ya kuzalisha Mbegu bora za kilimo.

Akizungumza na waandishi wa Habari Mkurugenzi Mtendaji Halmashauri ya Igunga Bi. Selwa Abdalah  amesema Baraza la Madiwani limeridhia kutoa shamba hilo lililokuwa likimilikiwa na Halmashauri ya Igunga.

“Hatua hii imefikia baada ya Waziri wa kilimo Mhe.Hussein Bashe akiwa katika ziara yake ya kikazi alitoa agizo kwa Halmashauri kutoa eneo la Uzalishaji wa Mbegu katika wilaya hiyo. Tayari Halmahshauri hiyo kupitia Baraza la Madiwani wametekeleza maagizo ya Waziri wa Kilimo kwa kutoa eneo lengo likiwa ni kuongeza Uzalishaji wa Mbegu na kupunguza muda na gharama za upatikanaji wa mbegu kwa wakulima wa Igunga, shamba hilo lipo katika Kijiji cha Bulyashiri kata ya Mwalala wilaya ya Igunga Mkoani Tabora. Amesema Bi. Selwa

Mkuu wa wilaya ya Igunga Bi. Sauda Mtondoo akikabidhi hati ya shamba hilo dhidi kwa Wakala wa Mbegu za kilimo ASA amesema, serikali ya Igunga itahakikisha inatoa ushirikiano wa kutosha kwa Wakala wa Mbegu katika hatua mbalimbali za Uzalishaji wa Mbegu.

Kwa upande wake Kaimu Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Mbegu za kilimo ASA Bwa. Leo Mavika ameipongeza Halmashauri ya wilaya ya Igunga kwa kutenga eneo hilo la Uzalishaji wa Mbegu Hekta 240.

“Shamba hili litawekewa miundombinu ya Umwagiliaji na kufungwa mitambo mbalimbali ya kisasa ya kuchakata Mbegu bora za kilimo tayari kuwafikia wananchi wa Igunga na Tanzania kwa Ujumla, pia litaongeza upatikanaji wa ajira mbalimbali kwa wananchi shambani na urahisi wa upatikanaji wa Mbegu pamoja na baadhi ya wakulima wanaolima jirani kupewa Mbegu bure kwa ajili ya kulinda ubora wa Mbegu. Amesema Bwa. Leo

Akimwakilisha Katibu Mkuu Wizara ya kilimo Mhandisi.Juma Mdeke amesema wizara ya kilimo imeishukuru Halmashauri ya Igunga kwa kukabidhi shamba hilo kwa ASA ambapo matarajio ni kuleta mchango mkubwa katika upatikanaji wa mbegu nchini.